Farida
Mangube, Morogoro
Katika maadhimisho ya Siku ya
Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kimeahidi kuendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili
wafanyakazi wake.
Akizungumza kwenye hafla fupi
iliyoandaliwa kwa ajili ya wafanyakazi wa SUA mara baada ya maadhimisho hayo,
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Fedha na Utawala, Amandus
Muhairwa, aliyemwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda, alisema
menejimenti ya SUA inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha changamoto hizo
zinapatiwa ufumbuzi.
“Tunatambua mchango wa wafanyakazi
na juhudi za viongozi wa vyama vya wafanyakazi chuoni hapa. Pia nawapongeza
waliopata tuzo za utendaji bora,” alisema Muhairwa, huku akiwahimiza
wafanyakazi kujitokeza kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba
2025.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama
cha Wafanyakazi wa RAAWU tawi la SUA, Bw. Faraja Kamendu, akisoma risala ya
wafanyakazi, aliushukuru uongozi wa Chuo kwa ushirikiano mzuri na kuwasihi
wafanyakazi kutimiza wajibu wao huku wakidumisha upendo wenye tija na kusimamia
nguzo ya umoja bila matabaka, akisisitiza kuwa mshikamano ni msingi wa
mafanikio.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha
Wafanyakazi THTU tawi la SUA, Dkt. Nickson Mkiramweni, aliwahimiza wafanyakazi
kujiunga na vyama vya wafanyakazi, akieleza kuwa kufanya hivyo kunaleta manufaa
makubwa katika kupigania haki na usawa mahali pa kazi.
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi
kwa mwaka 2025 yamebebwa na kaulimbiu isemayo: “Uchaguzi Mkuu 2025 Utuletee
Viongozi Wanaojali Haki na Maslahi ya Wafanyakazi – Sote Tushiriki.”






Comments
Post a Comment